Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 5:1-16

Matendo 5:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vilevile. Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume. Basi, Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!” Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari za tukio hilo waliogopa sana. Vijana wakafika, wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje, wakamzika. Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani. Petro akamwambia, “Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?” Yeye akamjibu, “Naam, ni kiasi hicho.” Naye Petro akamwambia, “Mbona mmekula njama kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako, sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia.” Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia, walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake. Hofu kubwa ikalikumba kanisa lote na wote waliosikia habari za tukio hilo. Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni. Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwaamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu. Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi. Hata watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kandokando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.

Shirikisha
Soma Matendo 5

Matendo 5:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akihifadhi kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuhifadhi kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu nyingi ikalipata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya. Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya mikeka na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makundi ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

Shirikisha
Soma Matendo 5

Matendo 5:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya. Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

Shirikisha
Soma Matendo 5

Matendo 5:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume. Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja, si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, je, fedha ulizozipata, si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.” Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakampeleka nje kumzika. Muda wa saa tatu baadaye, mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.” Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakupeleka nje.” Wakati ule ule, akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. Hofu kuu ikalipata kanisa lote, pamoja na watu wote waliosikia kuhusu matukio haya. Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.

Shirikisha
Soma Matendo 5