Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 5:1-16

Matendo 5:1-16 NENO

Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume. Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja, si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, je, fedha ulizozipata, si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.” Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakampeleka nje kumzika. Muda wa saa tatu baadaye, mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.” Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakupeleka nje.” Wakati ule ule, akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. Hofu kuu ikalipata kanisa lote, pamoja na watu wote waliosikia kuhusu matukio haya. Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.