Matendo 15:22-31
Matendo 15:22-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu. Wakawapa barua hii: “Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni nyinyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia. Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu. Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo, ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika. Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu: Msile vyakula vilivyotambikiwa vinyago; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!” Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua. Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana.
Matendo 15:22-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu. Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakateremka kwenda Antiokia; na baada ya kuwakusanya jamii yote wakawapa ile barua. Nao walipokwisha kuisoma wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
Matendo 15:22-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu. Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanya jamii yote wakawapa ile barua. Nao walipokwisha kuisoma wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
Matendo 15:22-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mitume na wazee, pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba, pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. Wakatumwa na barua ifuatayo: Sisi mitume na wazee, ndugu zenu. Kwa waumini wa Mataifa mlio Antiokia, Siria na Kilikia. Salamu. Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema. Kwaherini. Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua. Baada ya hao watu kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.