Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 15:22-31

Matendo 15:22-31 NENO

Mitume na wazee, pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba, pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. Wakatumwa na barua ifuatayo: Sisi mitume na wazee, ndugu zenu. Kwa waumini wa Mataifa mlio Antiokia, Siria na Kilikia. Salamu. Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema. Kwaherini. Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua. Baada ya hao watu kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.

Video ya Matendo 15:22-31