2 Wathesalonike 2:1-17
2 Wathesalonike 2:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja, tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule uasi utokee na yule Mwovu aonekane, ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. Yeye hujikuza yeye mwenyewe juu ya kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu; hata ataingia na kuketi ndani ya hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu. Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mngao wa kuja kwake. Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, bali wanafurahia dhambi, watahukumiwa. Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi ndugu, nyinyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara na kuzingatia yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua yetu. Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili muweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.
2 Wathesalonike 2:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ndugu, tunawasihini, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msishtushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa barua inayodhaniwa kuwa ni yetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama cha kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu. Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi niliwaambia hayo? Na sasa lizuialo mnalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inafanya kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hadi atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule mwasi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa dhihirisho la kuja kwake; kuja kwa yule mwasi ni kazi ya Shetani, atumiaye uwezo wote, ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu anawaletea upotevu mwingi, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli; aliyowaitia ninyi kwa Injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa barua yetu. Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.
2 Wathesalonike 2:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu. Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo? Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli; aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu. Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.
2 Wathesalonike 2:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho, wala neno la unabii, au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, kusema kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwepo. Mtu yeyote asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja hadi uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu. Je, hamkumbuki kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya? Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia. Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo hadi atakapoondolewa. Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. Kuja kwa yule mwasi kutalingana na vile Shetani hufanya kazi. Atatumia nguvu za aina mbalimbali katika miujiza, na ishara na ajabu za uongo, na katika njia zote ambazo uovu hudanganya wanaoangamia. Wanaangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli ili wapate kuokolewa. Kwa sababu hii, Mungu anawatumia nguvu ya udanganyifu, ili waamini uongo, na hivyo wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu. Lakini inatupasa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli. Kwa kusudi hili Mungu aliwaita ninyi kupitia Injili tuliyowahubiria, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua. Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.