2 Wakorintho 2:1-4
2 Wakorintho 2:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! Ndiyo maana niliwaandikia: Sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi. Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno.
2 Wakorintho 2:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini nafsini mwangu nilikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni. Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami? Nami niliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia. Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia nikiwa na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi.
2 Wakorintho 2:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini nafsini mwangu nalikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni. Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami? Nami naliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia. Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi.
2 Wakorintho 2:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi. Kwa kuwa nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha? Niliwaandikia hivyo ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao walipaswa kunifurahisha. Nilikuwa na uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu. Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana moyoni mwangu, tena kwa machozi mengi; shabaha yangu haikuwa niwahuzunishe, bali niwaoneshe kina cha upendo wangu kwenu.