Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 2:1-17

2 Wakorintho 2:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! Ndiyo maana niliwaandikia: Sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi. Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno. Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi, ila amewahuzunisha nyinyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. Kwa hiyo nawasihi: Mwonesheni kwamba mnampenda. Madhumuni yangu ya kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe, kama kweli ninacho cha kusamehe, nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo. Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia. Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.

2 Wakorintho 2:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini nafsini mwangu nilikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni. Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami? Nami niliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia. Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia nikiwa na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi. Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote. Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi; hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi. Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu. Maana niliandika kwa sababu hii pia, ili nipate wazi kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote. Lakini kama mkimsamehe mtu neno lolote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lolote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo, Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake. Basi nilipofika Troa kwa ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana, sikuona raha nafsini mwangu, kwa sababu sikumwona Tito ndugu yangu, bali niliagana nao, nikaondoka kwenda Makedonia. Ila Mungu ashukuriwe, anayetufanya tushangilie ushindi daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo? Kwa maana sisi si kama walio wengi, walichuuzao neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo.

2 Wakorintho 2:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini nafsini mwangu nalikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni. Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami? Nami naliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia. Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi. Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote. Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi; hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi. Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu. Maana naliandika kwa sababu hii pia, ili nipate bayana kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote. Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo, Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake. Basi nilipofika Troa kwa ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana, sikuona raha nafsini mwangu, kwa sababu sikumwona Tito ndugu yangu, bali niliagana nao, nikaondoka kwenda Makedonia. Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo? Kwa maana sisi si kama walio wengi, walighoshio neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo.

2 Wakorintho 2:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi. Kwa kuwa nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha? Niliwaandikia hivyo ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao walipaswa kunifurahisha. Nilikuwa na uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu. Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana moyoni mwangu, tena kwa machozi mengi; shabaha yangu haikuwa niwahuzunishe, bali niwaoneshe kina cha upendo wangu kwenu. Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote. Nasema hivi ili nisiwe mkali kupita kiasi. Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. Kwa hiyo, nawasihi mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwake. Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. Mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatujakosa kuzijua hila zake. Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango, bado nilikuwa sina amani kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao, nikaenda Makedonia. Lakini Mungu apewe shukrani, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye. Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo? Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na neno la Mungu ili tujifaidishe. Bali tunalinena neno lake kwa unyofu katika Kristo tukiwa mbele za Mungu, kama watu waliotumwa na Mungu.