Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 2:1-9 - Compare All Versions

2 Mambo ya Nyakati 2:1-9 BHN (Biblia Habari Njema)

Mfalme Solomoni alikata shauri kujenga nyumba ambamo Mwenyezi-Mungu ataabudiwa, na pia kujijengea yeye mwenyewe jumba la kifalme. Alipanga wanaume 70,000 wawe wachukuzi wa mizigo, 80,000 wawe wachonga mawe milimani na wengine 3,600 wawe wasimamizi wao. Kisha, Solomoni akatuma ujumbe kwa Hiramu, mfalme wa Tiro, akamwambia, “Nitendee na mimi kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, ulipompelekea mierezi ya kujengea ikulu. Tazama, karibu nianze kujenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Nitaiweka wakfu, nayo itakuwa mahali pa kufukiza ubani wa harufu nzuri mbele yake, na mahali pa mikate ya kuwekwa mbele yake daima, na tambiko za kuteketezwa asubuhi na jioni na pia siku za Sabato, mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo za Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyoiagiza Israeli milele. Nyumba ninayokusudia kujenga itakuwa kubwa sana, kwani Mungu wetu ni mkuu zaidi ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba ikiwa mbingu zenyewe hazimtoshi, wala mbingu za juu sana? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba isipokuwa tu kama mahali pa kufukizia ubani mbele yake? Basi, sasa nitumie mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu, fedha, shaba, na chuma, na nguo za rangi ya zambarau, za rangi nyekundu na ya samawati, ajuaye pia, kutia nakshi. Yeye atashirikiana katika kazi hiyo na mafundi walioko pamoja nami katika Yuda na Yerusalemu, ambao baba yangu Daudi aliwachagua. Tena nipelekee mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni, kwa maana najua ya kwamba watumishi wako ni hodari sana wa kupasua mbao huko Lebanoni. Nao watumishi wangu watashirikiana na watumishi wako, ili wanipasulie mbao kwa wingi, maana nyumba ninayokusudia kujenga ni kubwa na ya ajabu.

2 Mambo ya Nyakati 2:1-9 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba. Sulemani akahesabu watu elfu sabini wawe wapagazi, na watu elfu themanini wawe wachonga mawe milimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao. Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi. Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli. Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya pahali pa kufukizia mafusho mbele zake? Unitumie mtu stadi wa kuchonga dhahabu, fedha, shaba na chuma, na wa nguo za urujuani, nyekundu na samawati, ajuaye kutia nakshi, awe mmoja wa mastadi walioko pamoja nami Yuda na Yerusalemu ambao aliwaweka baba yangu Daudi. Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako, ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.

2 Mambo ya Nyakati 2:1-9 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba. Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao. Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi. Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli. Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake? Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu Daudi. Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako, ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.

2 Mambo ya Nyakati 2:1-9 NEN (Neno)

Sulemani akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe. Sulemani akaandika watu elfu sabini kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao. Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro: “Unitumie magogo ya mwerezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi. Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA Mungu wangu na kuliweka wakfu kwake kwa ajili ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate ya Wonesho kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamriwa za BWANA Mungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli. “Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kumtosha? Mimi ni nani basi hata nimjengee Hekalu, isipokuwa liwe tu mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake? “Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka. “Pia nitumie magogo ya mierezi, misunobari na misandali kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa.