Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 2:1-9

2 Nyakati 2:1-9 NEN

Sulemani akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe. Sulemani akaandika watu elfu sabini kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao. Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro: “Unitumie magogo ya mwerezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi. Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA Mungu wangu na kuliweka wakfu kwake kwa ajili ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate ya Wonesho kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamriwa za BWANA Mungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli. “Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kumtosha? Mimi ni nani basi hata nimjengee Hekalu, isipokuwa liwe tu mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake? “Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka. “Pia nitumie magogo ya mierezi, misunobari na misandali kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa.