1 Samueli 11:6-13
1 Samueli 11:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali. Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja. Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda. Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana. Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.” Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja. Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.” Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.”
1 Samueli 11:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Roho ya Mungu ikamjia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. Akachukua fahali wawili waliofungwa nira, akawakatakata vipande, kisha akawatuma wajumbe kuvipeleka vile vipande kote katika Israeli, wakisema, Yeyote ambaye hatamfuata Sauli na Samweli, ng'ombe wake watafanyiwa vivi hivi. Basi utisho wa BWANA ukawaangukia wale watu, wakatoka kwa pamoja. Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa elfu mia tatu, na Wayuda elfu thelathini. Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao wakafurahi. Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema. Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya kambi kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hadi wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja. Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue. Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israeli.
1 Samueli 11:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. Naye akatwaa jozi ya ng’ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng’ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa BWANA ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja. Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu. Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa. Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema. Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja. Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue. Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israeli.
1 Samueli 11:6-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira. Akachukua maksai wawili na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha kicho cha BWANA kikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja. Sauli alipowakusanya huko Bezeki, wanaume wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na wanaume wa Yuda elfu thelathini. Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni wanaume wa Yabesh-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipoenda na kutoa taarifa hii kwa wanaume wa Yabeshi, wakafurahi. Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.” Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja hadi mchana. Wale walionusurika wakatawanyika, hivi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja. Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatutawala?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.” Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii BWANA ameokoa Israeli.”