Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 11

11
Shauli anawashinda Waamoni
1Kisha mfalme Nahashi wa Waamoni, alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi. Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.” 2Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamngoa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.” 3Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.” 4Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti.
5Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi. 6Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali. 7Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja. 8Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda. 9Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana. 10Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.”
11Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja.
12Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.” 13Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.”
14Samueli akawaambia, “Twendeni wote Gilgali na kwa mara nyingine tutamtangaza Shauli kuwa mfalme.” 15Watu wote wakaenda Gilgali, na walipofika huko, wakamtawaza Shauli kuwa mfalme mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani hapo. Na Shauli pamoja na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samueli 11: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha