1 Samueli 11:1-5
1 Samueli 11:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha mfalme Nahashi wa Waamoni, alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi. Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.” Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamngoa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.” Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.” Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti. Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi.
1 Samueli 11:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupiga kambi juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia. Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hili mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kulia; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende kote mipakani mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutajisalimisha kwako. Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
1 Samueli 11:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia. Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang’olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea. Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
1 Samueli 11:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nahashi Mwamoni akakwea kuuzingira mji wa Yabesh-Gileadi kwa jeshi. Wanaume wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia.” Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitangʼoa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.” Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote. Ikies hakuna hata mmoja atayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.” Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa kuhusu masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa. Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza vile wanaume wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.