1 Petro 3:8-18
1 Petro 3:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, ajizuie asiseme mabaya aepe kusema uongo. Ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.” Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho
1 Petro 3:8-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la mwisho ni hili; muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme uongo. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana uko juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini hata mkiteswa kwa sababu ya kutenda haki, mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa heshima. Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho
1 Petro 3:8-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa
1 Petro 3:8-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, mkijaliana, na wanyenyekevu. Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. Kwa maana, “Yeyote apendaye uzima na kuona siku njema, basi auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila. Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema; lazima aitafute amani na kuifuatilia sana. Kwa maana macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza maombi yao. Bali uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu.” Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? Lakini hata ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki, mmebarikiwa. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” Bali mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao. Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, ikiwa ni mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu. Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho.