1 Petro 3:13-22
1 Petro 3:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.
1 Petro 3:13-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini hata mkiteswa kwa sababu ya kutenda haki, mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa heshima. Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiria; watu wasiotii hapo zamani, wakati Mungu alipowavumilia kwa subira, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yuko katika mkono wa kulia wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
1 Petro 3:13-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
1 Petro 3:13-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? Lakini hata ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki, mmebarikiwa. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” Bali mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao. Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, ikiwa ni mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu. Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho. Baada ya kufanywa hai, alienda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni: roho ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Nuhu, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika. Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu. Inatuokoa kupitia kwa ufufuo wa Yesu Kristo. Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote zimetiishwa chini yake.