1 Petro 1:8-12
1 Petro 1:8-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Nyinyi mnampenda, ingawaje hamjamwona, na mnamwamini, ingawa hammwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka, kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu. Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa. Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
1 Petro 1:8-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamumwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu. Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona.
1 Petro 1:8-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu. Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.
1 Petro 1:8-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha yenye utukufu na isiyoelezeka. Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu. Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewafikia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa. Walijaribu kujua ni wakati upi na ni mazingira yapi ambayo Roho wa Kristo, aliyekuwa ndani yao, alionesha alipotabiri mateso ya Kristo na utukufu ambao ungefuata. Walifunuliwa kwamba walikuwa wanawahudumia ninyi, bali si wao wenyewe, waliponena kuhusu mambo hayo. Mmeambiwa mambo haya sasa na wale waliowahubiria Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.