Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Petro 1:13-25

1 Petro 1:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga. Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu. Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi alivyo mtakatifu.” Mnapomtaja Mungu, nyinyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu. Maana mnajua kwamba nyinyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu. Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: Kwa fedha na dhahabu; bali kwa damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa. Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. Kwa njia yake, mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu. Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, nyinyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote. Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, nyinyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele. Kama Maandiko yasemavyo: “Kila binadamu ni kama majani, na utukufu wake wote ni kama ua la majani. Majani hunyauka na maua huanguka. Lakini neno la Bwana hudumu milele.” Neno hilo ni hiyo Habari Njema mliyohubiriwa.

Shirikisha
Soma 1 Petro 1

1 Petro 1:13-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa hiyo iweni tayari, na makini; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, nendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na dosari wala waa, yaani, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu; na kupitia kwake mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu. Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo safi. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, linalodumu hata milele. Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka; Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.

Shirikisha
Soma 1 Petro 1

1 Petro 1:13-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu. Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka; Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.

Shirikisha
Soma 1 Petro 1

1 Petro 1:13-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu. Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. Maana, “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni; majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Bwana ladumu milele.” Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

Shirikisha
Soma 1 Petro 1

1 Petro 1:13-25

1 Petro 1:13-25 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha