1 Petro 1:10-16
1 Petro 1:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa. Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu. Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga. Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu. Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi alivyo mtakatifu.”
1 Petro 1:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona. Kwa hiyo iweni tayari, na makini; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
1 Petro 1:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia. Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
1 Petro 1:10-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewafikia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa. Walijaribu kujua ni wakati upi na ni mazingira yapi ambayo Roho wa Kristo, aliyekuwa ndani yao, alionesha alipotabiri mateso ya Kristo na utukufu ambao ungefuata. Walifunuliwa kwamba walikuwa wanawahudumia ninyi, bali si wao wenyewe, waliponena kuhusu mambo hayo. Mmeambiwa mambo haya sasa na wale waliowahubiria Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya. Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”