1 Wakorintho 16:5-12
1 Wakorintho 16:5-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Nitakuja kwenu baada ya kupitia Makedonia – maana nataraji kupitia Makedonia. Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda. Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu. Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste. Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi. Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi. Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu. Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.
1 Wakorintho 16:5-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini nitakuja kwenu, nikiisha kupita kati ya Makedonia; maana napita kati ya Makedonia. Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha kokote nitakakokwenda. Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu natarajia kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia. Lakini nitakaa Efeso hadi siku ya Pentekoste; kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao. Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe; basi mtu yeyote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu. Lakini kuhusu Apolo, ndugu yetu, nilimsihi sana aje kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi.
1 Wakorintho 16:5-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini nitakuja kwenu, nikiisha kupita kati ya Makedonia; maana napita kati ya Makedonia. Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha ko kote nitakakokwenda. Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia. Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste; kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao. Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe; basi mtu ye yote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu. Lakini kwa habari za Apolo, ndugu yetu, nalimsihi sana aende kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi.
1 Wakorintho 16:5-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda. Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga. Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo. Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu. Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.