Zaburi 145:1-10
Zaburi 145:1-10 BHN
Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu; nitalitukuza jina lako daima na milele. Nitakutukuza kila siku; nitalisifu jina lako daima na milele. Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi; ukuu wake hauwezi kuchunguzika. Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa, watu watatangaza matendo yako makuu. Nitanena juu ya utukufu na fahari yako, nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu, nami nitatangaza ukuu wako. Watatangaza sifa za wema wako mwingi, na kuimba juu ya uadilifu wako. Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema; hakasiriki ovyo, amejaa fadhili. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote, ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza.