Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107:23-43

Zaburi 107:23-43 BHN

Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee. Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.

Soma Zaburi 107