Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107:23-43

Zaburi 107:23-43 NENO

Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu. Waliziona kazi za BWANA, matendo yake ya ajabu kilindini. Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu. Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini; katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka. Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao. Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono, mawimbi ya bahari yakatulia. Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee. Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zinazotiririka kuwa ardhi yenye kiu, nchi inayozaa ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo. Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zinazotiririka; aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi, Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua. Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni. Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia. Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo. Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao. Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa BWANA.