Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107:1-43

Zaburi 107:1-43 BHN

Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu, watu ambao aliwaokoa katika taabu, akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu, wasiweze kufikia mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu; wakavunjika moyo kabisa. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwaongoza katika njia iliyonyoka, mpaka wakaufikia mji wa kukaa. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huwatosheleza walio na kiu; na wenye njaa huwashibisha mema. Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma. Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao; chakula kikawa kinyaa kwao, wakawa nusura wafe. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Kwa neno lake aliwaponya, akawaokoa wasiangamie. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Wamtolee tambiko za shukrani; wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe. Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee. Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.

Soma Zaburi 107

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 107:1-43

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha