Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107:1-43

Zaburi 107:1-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu, watu ambao aliwaokoa katika taabu, akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu, wasiweze kufikia mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu; wakavunjika moyo kabisa. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwaongoza katika njia iliyonyoka, mpaka wakaufikia mji wa kukaa. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huwatosheleza walio na kiu; na wenye njaa huwashibisha mema. Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma. Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao; chakula kikawa kinyaa kwao, wakawa nusura wafe. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Kwa neno lake aliwaponya, akawaokoa wasiangamie. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Wamtolee tambiko za shukrani; wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe. Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee. Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.

Shirikisha
Soma Zaburi 107

Zaburi 107:1-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitangatanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na minyororo, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye Juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akaivunja minyororo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba. Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, Hao huziona kazi za BWANA, Na maajabu yake vilindini. Maana alisema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi ya bahari. Walirushwa juu mbinguni, waliteremka hadi vilindini, Uhodari wao ukayeyuka katika maafa yao. Waliyumbayumba, walipepesuka kama mlevi, Ujuzi wao wote uliwaishia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye akawaleta mpaka bandani waliyoitamani. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza la wazee. Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi kavu. Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wamejenga mji wa kukaa. Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. Naye aliwabariki wakaongezeka sana, Wala hawapunguzi mifugo wao. Walipopungua na kudhilika, Kwa kuonewa na dhiki na huzuni. Aliwamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. Lakini alimwinua mhitaji juu mbali na mateso, Na kuwaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Wanyofu wa moyo wanaona na kufurahi, Na waovu wote wananyamazishwa. Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za BWANA.

Shirikisha
Soma Zaburi 107

Zaburi 107:1-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba. Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, Hao huziona kazi za BWANA, Na maajabu yake vilindini. Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake. Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya. Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee. Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu. Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa. Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa. Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao. Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni. Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo. Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa. Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za BWANA.

Shirikisha
Soma Zaburi 107

Zaburi 107:1-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mshukuruni BWANA, kwa kuwa yeye ni mwema, upendo wake wadumu milele. Waliokombolewa wa BWANA na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui, wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi. Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema. Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, kwa sababu walikuwa wameasi dhidi ya maneno ya Mungu na kudharau shauri la Aliye Juu Sana. Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwepo yeyote wa kuwasaidia. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma. Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao. Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizo yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha. Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu. Waliziona kazi za BWANA, matendo yake ya ajabu kilindini. Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu. Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini, katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka. Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao. Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono, mawimbi ya bahari yakatulia. Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee. Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zitiririkazo kuwa ardhi yenye kiu, nchi izaayo ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo. Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zitiririkazo; aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi, Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua. Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni. Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia. Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo. Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao. Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa BWANA.

Shirikisha
Soma Zaburi 107

Zaburi 107:1-43

Zaburi 107:1-43 BHNZaburi 107:1-43 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha