Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 24:13-35

Luka 24:13-35 BHN

Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.” Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.” Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.

Soma Luka 24

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha