Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 59

59
Nabii azilaani dhambi za watu
1Msifikiri mkono wa Mungu ni mfupi,
hata asiweze kuwaokoeni;
au masikio yake yamezibika,
hata asiweze kuwasikieni.
2Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu wenu,
dhambi zenu zimemfanya ajifiche mbali nanyi
hata asiweze kuwasikieni.
3Maana mikono yenu imetiwa najisi kwa mauaji,
na vidole vyenu kwa matendo maovu.
Midomo yenu imesema uongo,
na ndimi zenu husema uovu.
4Hakuna atoaye madai yake kwa haki,
wala anayeshtaki kwa uaminifu.
Mnategemea hoja batili;
mnasema uongo.
Mnatunga hila na kuzaa uovu.
5Mnaangua mayai ya joka lenye sumu,
mnafuma utando wa buibui.
Anayekula mayai yenu hufa,
na yakipasuliwa nyoka hutokea.
6Utando wenu haufai kwa mavazi,
watu hawawezi kujifunikia mnachofuma.
Kazi zenu ni kazi za uovu,
matendo yenu yote ni ukatili mtupu.
7 #59:7-8 Taz Rom 3:15-17 Mko mbioni kutenda maovu,
mnaharakisha kumwaga damu isiyo na hatia.
Mawazo yenu ni mawazo ya uovu,
popote mwendapo mnaacha ukiwa na uharibifu.
8Njia ya amani hamwijui kamwe;
njia zenu zote ni za dhuluma.
Mmejifanyia njia potovu,
yeyote anayepitia humo hapati amani.
Watu wanakiri dhambi yao
9Ndio maana haki iko mbali nasi,
maongozi ya uadilifu hayapo kwetu.
Tunatazamia kupata mwanga kumbe ni giza tupu,
twatazamia mwangaza, lakini twatembea gizani.
10Kama vipofu twapapasapapasa ukuta;
tunasitasita kama watu wasio na macho.
Tunajikwaa mchana kana kwamba ni usiku,
miongoni mwa wenye nguvu sisi ni kama wafu.
11Twanguruma kama dubu,
twaomboleza tena na tena kama hua.
Twatazamia hukumu ya haki, lakini haipo,
twatazamia wokovu, lakini uko mbali nasi.
12Makosa yetu mbele yako ni mengi mno,
dhambi zetu zashuhudia dhidi yetu.
Naam, makosa yetu tunaandamana nayo,
tunayajua maovu yetu.
13Tumekuasi na kukukana ee Mwenyezi-Mungu,
tumekataa kukufuata ewe Mungu wetu.
Udhalimu na uasi ndivyo tunavyopania,
mioyoni mwetu twatunga na kutoa maneno ya uongo.
14Haki imewekwa kando,
uadilifu uko mbali;
ukweli unakanyagwa mahakamani,
uaminifu haudiriki kuingia humo.
15Ukweli umekosekana,
naye anayeacha uovu hunyanyaswa.
Mungu ajiandaa kuwakomboa watu wake
Mungu aliona mambo hayo, akachukizwa,
alichukizwa kwamba hakuna haki.
16Aliona kwamba hakuna mtu aliyejali,
akashangaa kwamba hakuna aliyeingilia kati.
Basi akaamua kunyosha mkono wake mwenyewe,
uadilifu wake ukamhimiza.
17Alivaa uadilifu kama vazi la kujikinga kifuani,
na wokovu kama kofia ya chuma kichwani.
Atajivika kisasi kama vazi,
na kujifunika wivu kama joho.
18Atawaadhibu maadui kadiri ya matendo yao,
naam, ghadhabu yake na kisasi vitawapata maadui zake;
atawaadhibu hata wakazi wa nchi za mbali.
19Toka magharibi hadi mashariki,
kila mtu atamcha Mwenyezi-Mungu
na kutambua utukufu wake.
Maana atakuja kama mto uendao kasi,
mto unaosukumwa kwa upepo wa Mwenyezi-Mungu.
20Naye atakuja Siyoni kama Mkombozi,
Mkombozi wa wazawa wa Yakobo
ambao wataachana na makosa yao.
Asema Mwenyezi-Mungu.
21Mwenyezi-Mungu asema:
“Mimi nafanya nanyi agano hili:
Roho yangu niliyowajazeni,
maneno niliyoyaweka mdomoni mwenu,
hayataondoka kwenu kamwe,
wala kwa watoto na wajukuu zenu,
tangu sasa na hata milele.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 59: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha