Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 48

48
Mungu atangaza matukio mapya
1Sikilizeni, enyi watu wa Yakobo,
enyi mnaojulikana kwa jina la Israeli,
nyinyi mlio wa ukoo wa Yuda.
Nyinyi huapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu,
na kudai mnamwabudu Mungu wa Israeli;
lakini hayo si ukweli wala sawa.
2Nyinyi mnaona fahari kujiita watu wa mji mtakatifu,
na kujidai kumtegemea Mungu wa Israeli,
ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
3“Nilitangaza zamani matukio ya awali,
niliyatamka mimi mwenyewe
na kuyafanya yajulikane kwenu.
Mara nikaanza kuyatekeleza,
nayo yakapata kutukia.
4Lakini nilikujua wewe kuwa mkaidi;
kichwa kigumu kama chuma,
uso wako mkavu kama shaba.
5Kwa hiyo nilikutangazia tangu zamani,
kabla hayajatukia mimi nilikutangazia,
usije ukasema, ‘Kinyago changu kiliyatenda hayo,
sanamu zangu za kuchonga na kusubu ziliyafanya.’
6“Wewe uliyasikia na sasa unayaona yote.
Kwa nini huwezi kuyakiri?
Tangu sasa nitakujulisha mambo mapya;
mambo yaliyofichika ambayo hukuyajua.
7Mambo hayo yanatukia sasa;
hukupata kuyasikia kabla ya leo,
hivyo huwezi kusema, ‘Aa! Nilikwisha yajua.’
8Hujapata kamwe kuyasikia wala kuyajua;
tangu zamani masikio yako hayakuyasikia.
Nilijua kuwa wewe ni mwenye hila,
na kwamba wewe ni mwasi tangu kuzaliwa.
9“Kwa heshima ya jina langu,
ninaiahirisha hasira yangu;
kwa ajili ya heshima yangu,
ninaizuia nisije nikakuangamiza.
10Mimi nitawajaribu lakini si kama fedha katika tanuri.
Nitawajaribu katika tanuri ya taabu.
11Ninafanya hivyo kwa ajili yangu mwenyewe.
Kwa nini jina langu lidharauliwe?
Utukufu wangu siwezi kumpa mwingine!
Koreshi, mteule wa Mwenyezi-Mungu
12 #48:12 Taz Isa 44:6; Ufu 1:17, 22:13 “Nisikilize ee taifa la Yakobo,
nisikilize ee Israeli niliyekuita.
Mimi ndiye Mungu;
mimi ni wa kwanza na wa mwisho.
13Kwa mkono wangu niliuweka msingi wa dunia,
mimi mwenyewe nilizitandaza mbingu.
Nikiziita mbingu na dunia,
zinasimama haraka mbele yangu.
14“Kusanyikeni nyote msikilize!
Nani kati ya miungu yenu aliyetabiri vitu hivi?
Mimi Mwenyezi-Mungu nampenda Koreshi;
yeye atatekeleza lengo langu kuhusu Babuloni,
naam, yeye atawashambulia Wakaldayo.
15Mimi, naam, mimi nimeyasema na kumwita;
nimemleta, naye atafaulu katika mpango wake.
16Njoni karibu nami msikie jambo hili:
Tangu mwanzo mimi sikusema kwa siri,
tangu mambo hayo yaanze kutendeka, nimekuwapo.”
Sasa, Bwana Mungu amenituma,
na kunipa nguvu ya roho yake.#48:16 Sasa … roho wake: Maneno haya hayaonyeshi dhahiri ni nani anayesema; Pengine ni rafiki (Koreshi) aliyetajwa katika aya ya 14.
Mpango wa Mungu kwa watu wake
17Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli,
Mkombozi wako, asema hivi:
“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
ninayekufundisha kwa faida yako,
ninayekuongoza katika njia unayotakiwa kwenda.
18Laiti ungalizitii amri zangu!
Hapo baraka zingekutiririkia kama mto,
ungepata fanaka kwa wingi kama mawimbi ya bahari.
19Wazawa wako wangekuwa wengi kama mchanga,
naam, wangekuwa wengi kama chembe za mchanga.
Jina lao kamwe lisingaliondolewa,
kumbukumbu lao halingalitoweka mbele yangu.”
20 #48:20 Taz Ufu 18:4 Sasa, ondokeni Babuloni!
Kimbieni kutoka Kaldayo!
Tangazeni jambo hili kwa sauti za shangwe,
enezeni habari zake kila mahali duniani.
Semeni: “Mwenyezi-Mungu amelikomboa
taifa la mtumishi wake Yakobo.”
21Alipowaongoza jangwani hawakuona kiu,
aliwatiririshia maji kutoka mwambani,
aliupasua mwamba maji yakabubujika.
22 #48:22 Taz Isa 57:21 Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu waovu sitawapa amani.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 48: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha