Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 24:1-15

Isaya 24:1-15 BHN

Sasa Mwenyezi-Mungu anaiharibu dunia na kuifanya tupu. Atausokota uso wa dunia na kuwatawanya wakazi wake. Kila mtu atapatwa na mambo yaleyale: Mtu wa kawaida na kuhani; mtumwa na bwana wake; mjakazi na bibi yake; mnunuzi na mwuzaji; mkopeshaji na mkopaji; mdai na mdaiwa. Dunia itaharibiwa kabisa na kuangamizwa; Mwenyezi-Mungu ametamka hayo. Dunia inakauka na kunyauka; ulimwengu unafadhaika na kunyauka; mbingu zinafadhaika pamoja na dunia. Watu wameitia najisi dunia maana wamezivunja sheria za Mungu, wamezikiuka kanuni zake, wamelivunja agano lake la milele. Kwa sababu hiyo laana inaitokomeza dunia, wakazi wake wanateseka kwa makosa yao. Wakazi wa dunia wamepungua, ni watu wachache tu waliosalia. Mizabibu inanyauka, divai inakosekana. Wote waliokuwa wenye furaha sasa wanasononeka kwa huzuni. Mdundo wa vigoma umekoma, nderemo na vifijo vimetoweka; midundo ya vinubi imekomeshwa. Hakuna tena kunywa divai na kuimba; mvinyo umekuwa mchungu kwa wanywaji. Mji uliohamwa umejaa uharibifu; kila nyumba imefungwa asiingie mtu. Kuna kilio barabarani kwa kukosa divai; shangwe yote imekoma, furaha imetoweka duniani. Mji ni magofu matupu; malango yake yamevunjwavunjwa. Kama vile zeituni chache tu juu ya mzeituni au tini chache tu juu ya mtini baada ya kumaliza mavuno, ndivyo itakavyokuwa katika nchi zote: Watu wachache watabakia hai. Watakaosalia watapaza sauti, wataimba kwa shangwe. Kutoka magharibi watatangaza ukuu wa Mwenyezi-Mungu, nao wakazi wa mashariki watamsifu. Watu wa mbali watalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

Soma Isaya 24