Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 24:1-15

Isaya 24:1-15 NENO

Tazama, BWANA ataifanya dunia kuwa ukiwa na kuiharibu, naye atauharibu uso wake na kutawanya wanaoishi ndani yake: ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mjakazi wake, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai. Dunia itaharibiwa kabisa na kutekwa nyara kabisa. BWANA amesema neno hili. Dunia inakauka na kunyauka, dunia inanyongʼonyea na kunyauka, waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea. Dunia imetiwa unajisi na watu wake; wameacha kutii sheria, wamevunja amri na kuvunja agano la milele. Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia, watu wake lazima waichukue hatia yao. Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa, nao waliosalia ni wachache sana. Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka, watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni. Furaha ya matoazi imekoma, kelele za wenye furaha zimekoma, shangwe za kinubi zimenyamaza. Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake. Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa. Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia. Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande. Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa. Wanapaza sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa BWANA. Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni BWANA utukufu, liadhimisheni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.