Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 5:1-20

Waefeso 5:1-20 BHN

Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. Basi, msishirikiane nao. Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga, maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki katika matendo yasiyofaa ya giza, bali yafichueni. Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. Lakini kila kitu kikifichuliwa na mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: “Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangaza.” Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi. Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waefeso 5:1-20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha