Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 5:1-20

Waefeso 5:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. Basi, msishirikiane nao. Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga, maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki katika matendo yasiyofaa ya giza, bali yafichueni. Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. Lakini kila kitu kikifichuliwa na mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: “Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangaza.” Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi. Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Shirikisha
Soma Waefeso 5

Waefeso 5:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hivyo mwigeni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali kuwepo kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, (ndiye mwabudu sanamu), aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; nendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini chochote kinachoangazwa na nuru hudhihirishwa, maana chochote kile kilichoadhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana nyakati hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo.

Shirikisha
Soma Waefeso 5

Waefeso 5:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo

Shirikisha
Soma Waefeso 5

Waefeso 5:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu. Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii. Kwa hiyo, msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini. Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana, kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana: “Amka, wewe uliyelala, ufufuke kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangazia.” Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Shirikisha
Soma Waefeso 5

Waefeso 5:1-20

Waefeso 5:1-20 BHNWaefeso 5:1-20 BHNWaefeso 5:1-20 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha