Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11 BHN

“Kila mwisho wa mwaka wa saba mtawasamehe wadeni wenu wote. Hivi ndivyo mtakavyofanya: Kila mmoja aliyemkopesha jirani yake, alifute hilo deni, wala asijaribu kumdai kwa sababu Mwenyezi-Mungu mwenyewe ameamua deni hilo lifutwe. Mnaweza kuwadai wageni, lakini madeni yote ya ndugu zenu wenyewe mtayafuta. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika nchi anayowapa iwe mali yenu. Hakuna hata mmoja atakayekuwa maskini kati yenu, mradi tu mumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kufuata kwa uangalifu amri ninazowapeni hivi leo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama vile alivyowaahidi. Nanyi mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Kadhalika mtatawala mataifa mengi, lakini mataifa hayo hayatawatawala nyinyi. “Kukiwa na maskini wa jamaa yenu katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu atawapa, msiwe wachoyo na wagumu kwake. Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake. Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu. Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo. Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha