2 Wakorintho 6:1-13

BHN
Biblia Habari Njema

1Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. 2Mungu asema hivi:
“Wakati wa kufaa nimekusikiliza,
wakati wa wokovu nikakusaidia.”
Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu!
3Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote. 4Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: Kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. 5Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. 6Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, 7kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu kila upande. 8Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; 9kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote; kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni hai kabisa. 10Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini, twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.
11Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. 12Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu nyinyi wenyewe, na si kwa upande wetu. 13Sasa nasema nanyi kama watoto wangu: Wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.