1 Samueli 3:2-10
1 Samueli 3:2-10 BHN
Siku moja usiku, Eli ambaye macho yake yalikuwa yamefifia, alikuwa amelala katika chumba chake. Samueli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu karibu na sanduku la agano la Mungu. Taa ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa bado inawaka kwani kulikuwa hakujapambazuka. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli! Naye Samueli, akaitika, “Naam!” Kisha Samueli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia, “Nimekuja kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Mimi sijakuita. Nenda ukalale.” Samueli akarudi na kulala. Mwenyezi-Mungu akamwita tena, “Samueli!” Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Sikukuita mwanangu, kalale tena.” Samueli alikuwa hamjui Mwenyezi-Mungu bado, wala ujumbe wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado haujafunuliwa kwake. Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli kwa mara ya tatu. Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Ndipo Eli alipotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemwita Samueli. Kwa hiyo Eli akamwambia Samueli, “Nenda ukalale, na akikuita, mwambie hivi: ‘Sema, ee Mwenyezi-Mungu, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.’” Hivyo Samueli akarudi na kulala mahali pake. Baadaye Mwenyezi-Mungu akaja na kusimama hapo, akamwita Samueli kama hapo awali, “Samueli! Samueli!” Samueli akasema, “Sema, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.”