Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 9:1-29

Warumi 9:1-29 SRUV

Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyoisha moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazawa wa Abrahamu, bali, Katika Isaka wazawa wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazawa. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atapata mtoto wa kiume. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? La hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu. Kwa maana Maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nioneshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake? La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwa nini umeniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima? Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyokuwa karibu kuharibiwa; tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu; ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia? Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na kumwita mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai. Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema, Hesabu ya wana wa Israeli, ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari, ni mabaki yao tu watakaookolewa. Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata. Tena kama Isaya alivyotangulia kunena, Kama Bwana wa majeshi asingalituachia uzao, Tungalikuwa kama Sodoma, tungalifananishwa na Gomora.

Soma Warumi 9

Video ya Warumi 9:1-29