Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 19:1-14

Zaburi 19:1-14 SRUV

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa. Hakuna usemi wala maneno, Sauti yao haisikilikani. Sauti yao imeenea duniani kote, Na maneno yao hadi miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema, Nalo hutokeza kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake. Kuchomoza kwake ni katika mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake ni hadi miisho ya mbingu, Wala hakuna kitu Kisichofikiwa na joto lake. Sheria ya BWANA ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa BWANA ni amini, Humtia hekima mtu asiye nayo. Maagizo ya BWANA ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, Huyatia macho nuru. Kicho cha BWANA ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za BWANA ni kweli, Zina haki kabisa. Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali. Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu kuu. Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.

Soma Zaburi 19

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 19:1-14

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha