Hesabu 29:1-11
Hesabu 29:1-11 SRUV
Tena mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yoyote ya utumishi; ni siku ya kupiga tarumbeta kwenu. Nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng'ombe dume mchanga mmoja, na kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume saba wa mwaka mmoja wote wasiwe na dosari; pamoja na sadaka yake ya unga, unga laini uliochanganywa na mafuta, sehemu ya tatu ya kumi ya ng'ombe, sehemu ya mbili ya kumi kwa kondoo dume, na sehemu ya moja ya kumi kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya kuandama mwezi, na sadaka yake ya unga, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kama ilivyo amri yake, kuwa harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto. Tena siku ya kumi ya huo mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; nanyi mtajinyima nafsi zenu, msifanye kazi yoyote ya utumishi lakini mtamsogezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza; ng'ombe dume mchanga mmoja, na kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume saba wa mwaka mmoja; watakuwa wakamilifu kwenu; pamoja na sadaka zake za unga, unga laini uliochanganywa na mafuta, sehemu ya tatu ya kumi kwa huyo ng'ombe, na sehemu ya mbili ya kumi kwa huyo kondoo, na sehemu ya moja ya kumi kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya dhambi ya upatanisho, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji.