Luka 5:1-4, 6-11
Luka 5:1-4 SRUV
Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona mashua mbili zimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika mashua moja, ndiyo yake Simoni, akamtaka aipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano akiwa katika mashua. Na alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.
Luka 5:6-11 SRUV
Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washiriki wenzao waliokuwa katika mashua nyingine, waje kuwasaidia; wakaja, wakazijaza mashua zote mbili, hata zikakaribia kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini mbele ya Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki waliowapata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuziegesha mashua zao pwani, wakaacha vyote wakamfuata.