Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mambo ya Walawi 16:14-30

Mambo ya Walawi 16:14-30 SRUV

Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba. Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. Kisha atatoka na kwenda katika madhabahu iliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke. Naye akiisha kufanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, na hema ya kukutania, na madhabahu, atamleta yule mbuzi aliye hai. Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, na dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atapelekwa jangwani na mtu aliyetayarishwa kwa ajili ya kazi hiyo Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyokaliwa na watu; kisha atamwacha aende jangwani. Na Haruni ataingia katika hema ya kukutania, naye atavua mavazi yake ya kitani, aliyoyavaa alipoingia katika patakatifu, atayaacha humo; naye ataosha mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na kuvaa nguo zake, na kutoka, na kusongeza sadaka ya kuteketezwa yake mwenyewe, na sadaka ya kuteketezwa ya watu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu. Na mafuta ya sadaka ya dhambi atayateketeza juu ya madhabahu. Na mtu yule amwachaye mbuzi wa Azazeli aende zake, ataosha nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia katika kambi. Na yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, na yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, ambao damu yao ililetwa ndani ifanye ukumbusho katika patakatifu, watachukuliwa nje ya kambi; nao watateketeza ngozi zao, na nyama yao, na mavi yao. Na yeye awachomaye moto atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia kambini. Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajinyima, msifanye kazi ya namna yoyote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu. Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za BWANA.