Yoshua 6:10-20
Yoshua 6:10-20 SRUV
Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lolote lisitoke kinywani mwenu, hadi siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa humo kambini. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA. Na wale makuhani saba wakayachukua mabaragumu saba ya pembe za kondoo dume mbele ya sanduku la BWANA, wakaenda huku wakiyapiga mabaragumu; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; huku makuhani wakiyapiga mabaragumu bila kukoma. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tu ambapo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani wakayapiga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtaifanya kambi ya Israeli kuwa imelaaniwa na kuifadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji.