Yoshua 6:10-20
Yoshua 6:10-20 NENO
Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” Basi akalipeleka Sanduku la BWANA kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala. Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la BWANA. Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la BWANA wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la BWANA, huku baragumu hizo zikiendelea kulia. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita. Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa BWANA kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu. Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina yake.” Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.