Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 42

42
Yeremia awashauri walionusurika wasihame
1 # Yer 40:8,13; 41:11 Ndipo makamanda, wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia, 2#Kut 8:28; 1 Sam 7:8; 1 Fal 13:6; Isa 37:4; Yer 21:2; Mdo 8:24; Yak 5:16; Law 26:22 wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa BWANA, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo; 3#Ezr 8:21; Zab 27:11; Mit 3:5,6 ili kwamba BWANA, Mungu wako, atuoneshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende. 4#1 Fal 22:14; 1 Sam 3:18; Mdo 20:20 Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba BWANA, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lolote ambalo BWANA atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote. 5Wakamwambia Yeremia, BWANA na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo BWANA, Mungu wako, atakutuma utuletee. 6#Mwa 31:50; Kum 6:3; Yer 7:23 Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya BWANA, Mungu wetu.
7Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. 8Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, 9akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi; 10#Yer 24:6; 31:28; 18:8; Kum 32:36 Ikiwa mtabaki katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang'oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda. 11#Hes 14:9; Kum 20:4; Zab 46:7; Isa 43:5; Rum 8:31 Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya kutoka kwa mkono wake. 12#Zab 106:45,46 Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe. 13#Yer 44:16 Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya BWANA, Mungu wenu; 14mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko; 15#Kum 17:16; Lk 9:51 basi, lisikieni neno la BWANA, enyi mabaki ya Yuda; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mnakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko; 16#Eze 11:8 basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko. 17#Yer 24:10; 44:14,28 Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hakuna mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao. 18#2 Nya 34:25; Yer 6:11; Eze 22:22; Yer 18:16; 24:9; 26:6 Maana BWANA wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena. 19#Kum 17:16 BWANA asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo. 20Maana mmetenda kwa hila juu ya nafsi zenu wenyewe; kwa kuwa mmenituma kwa BWANA, Mungu wenu, mkisema, Utuombee kwa BWANA, Mungu wetu, ukatufunulie sawasawa na yote atakayoyanena BWANA, Mungu wetu, nasi tutayatenda; 21#Zek 7:11 nami nimewafunulia haya leo; lakini ninyi hamkuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu, katika neno lolote ambalo amenituma kwenu. 22#Eze 6:11 Basi, sasa jueni sana ya kuwa mtakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, katika mahali pale mnapopatamani kwenda na kukaa.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 42: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha