Isaya 49:8-26
Isaya 49:8-26 SRUV
BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; joto halitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia zangu zote kuu zitainuliwa. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika hao wote kama pambo, nawe utajipamba kwao kama bibi arusi. Maana kuhusu mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami niko peke yangu, nimehamishwa, ninatangatanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, niliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi? Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwainulia makabila ya watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao. Na wafalme watakuwa baba zako walezi, na malkia zao mama zako walezi; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika. Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka wake, au mateka wa mtu katili kuokoka? Naam, BWANA asema hivi, Hata mateka wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka wake aliye katili wataokoka; kwa maana nitapambana na yeye abishanaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na watu wote watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.