Isaya 26:1-10
Isaya 26:1-10 SRUV
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Fungueni malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hadi chini, auleta hadi mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa BWANA.


