Hosea 13:7-16
Hosea 13:7-16 SRUV
Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani; nitawajia kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua. Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, kwa kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako. Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu? Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu. Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba. Uchungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto. Nitawakomboa kwa nguvu za kaburi; nitawaokoa kutoka kwa mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Huruma itafichika machoni mwangu. Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya BWANA itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo. Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatumbuliwa.