Hosea 13:7-16
Hosea 13:7-16 NENO
Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba, kama chui nitawavizia kando ya njia. Kama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, nitawashambulia na kurarua vifua vyenu. Kama simba nitawala; mnyama pori atawararua vipande vipande. “Ee Israeli, umeangamizwa, kwa sababu wewe u kinyume nami, kinyume na msaidizi wako. Yuko wapi mfalme wako, ili apate kukuokoa? Wako wapi watawala wako katika miji yako yote ambao ulisema kuwahusu, ‘Nipe mfalme na wakuu’? Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme na katika ghadhabu yangu nilimwondoa. Kosa la Efraimu limehifadhiwa, dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu. Uchungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia, lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima; wakati utakapowadia hatatoka katika tumbo la mama yake. “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi, nitawakomboa kutoka mautini. Yako wapi, ee mauti, mateso yako? Uko wapi, ee Kuzimu, uharibifu wako? “Sitakuwa na huruma, hata ingawa Efraimu atastawi miongoni mwa ndugu zake. Upepo wa mashariki kutoka kwa BWANA utakuja, ukivuma kutoka jangwani, chemchemi yake haitatoa maji na kisima chake kitakauka. Ghala lake litatekwa hazina zake zote. Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao, kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao. Wataanguka kwa upanga; watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini, wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”