Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 31:1-16

Mwanzo 31:1-16 SRUV

Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama hapo awali. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. Yakobo akatuma watu ili kuwaita Raheli na Lea waje malishoni kwenye mifugo wake. Akawaambia, Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwachia anidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, niliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda kondoo wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutenda Labani. Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa. Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je, Imebakia sehemu au urithi kwa ajili yetu katika nyumba ya baba yetu? Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa? Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi, yoyote Mungu aliyokuambia, uyafanye.

Soma Mwanzo 31