Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 6

6
Amri kuu
1Na hii ndiyo sheria, amri na hukumu, alizoziamuru BWANA, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayovuka kuimiliki; 2#Kut 20:2-20; Zab 111:10; 128:1; Mhu 12:13; Mit 3:1 upate kumcha BWANA, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. 3Sikiliza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.
4 # Mk 12:29; Isa 9:6; Yn 1:1; 10:30; 17:3; 1 Kor 8:4; Efe 4:6; Flp 2:5,6 Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja#6:4 Au Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; au Bwana Mungu wetu ni mmoja; au Bwana ni Mungu wetu, Bwana ni mmoja. 5#Mt 22:37; Mk 12:30-32; Lk 10:27; Kum 30:6; 1 Yoh 5:3 Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6#Kum 11:18-20; Isa 51:7 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; 7#Efe 6:4 nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyasema uishipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. 8#Mit 6:21; Kut 13:9; Mit 3:3; 7:3 Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. 9#Kum 11:20; Isa 50:8; 57:8 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.
Hadhari ya kutotii
10 # Mwa 12:7; 26:3; 28:13; Yos 24:13; Zab 105:44 Kisha BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Abrahamu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, 11na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vilivyochimbwa usivyochimba wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; 12ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. 13#Mt 4:10; Lk 4:8; Kum 13:4; Zab 63:11 Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. 14#Yer 25:6 Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; 15kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.
16 # Kut 17:1-7; Mt 4:7; Lk 4:12; 1 Kor 10:9 Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. 17#Zab 119:4 Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na maagizo yake, na amri zake alizokuagiza. 18Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako, 19ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA.
20Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, Ni nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu? 21Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; 22BWANA akaonesha ishara na maajabu makubwa na mazito, juu ya Misri, Farao, na nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; 23akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia babu zetu. 24#Ayu 35:7,8; Yer 32:39; Zab 41:2; Lk 10:28 BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. 25#Rum 10:3 Tena itakuwa haki kwetu, tukizingatia kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu la Torati 6: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha