Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 13:13-25

Matendo 13:13-25 SRUV

Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Kisha, baada ya Torati na kitabu cha Manabii kusomwa, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa, lisemeni. Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi Waisraeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza. Na kwa muda wa miaka kama arubaini akawavumilia katika jangwa. Na alipokwisha kuwaangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini; baada ya hayo akawapa waamuzi hata wakati wa nabii Samweli. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila la Benyamini, kwa muda wa miaka arubaini. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiria watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mnadhani mimi ni nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.

Soma Matendo 13

Video ya Matendo 13:13-25