Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zab 18:21-50

Zab 18:21-50 SUV

Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo. Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu. Mradi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili. Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; BWANA Mungu wangu aniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya BWANA imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu ila BWANA? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu? Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kuume umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza. Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe. Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu. Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali. Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita BWANA lakini hakuwajibu, Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani. Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake hata milele.

Soma Zab 18

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zab 18:21-50

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha