Zab 119:129-176
Zab 119:129-176 SUV
Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika. Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga. Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako. Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki. Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako. Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako. Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili. Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi. Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako. Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda. Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako. Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli. Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu. Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi. Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee BWANA, uitike; Nitazishika amri zako. Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako. Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini. Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako. Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee BWANA, unihuishe sawasawa na hukumu yako. Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako. Ee BWANA, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli. Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele. Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako. Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako. Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako. Ee BWANA, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako. Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako. Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako. Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee BWANA, unihuishe sawasawa na fadhili zako. Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele. Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako. Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi. Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda. Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako. Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza. Ee BWANA, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda. Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno. Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako. Ee BWANA, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako. Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako. Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako. Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki. Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako. Ee BWANA, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu. Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie. Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.